Mwenyekiti wa chama cha ACT
wazalendo, Zitto Kabwe amezungumzia hatua ya Profesa Kitila Mkumbo kuwa Katibu
Mkuu wizara ya Maji na Umwagiliaji.
Amesema kuwa chama hicho kimepokea kwa
mikono miwili uteuzi huo huku akisema kuwa Profesa Kitila ameandika barua ya
kujiuzulu nafasi yake ya mshauri wa Chama na kubaki kuwa mwanachama wa kawaida
tu.
Leo asubuhi Rais John Pombe Magufuli
amemteua Mshauri wa Chama chetu Prof. Kitila Mkumbo kuwa Katibu Mkuu wa Wizara
ya Maji na Umwagiliaji.
Kupitia Facebook Mheshimiwa Zitto
ameandika:
Uteuzi wa
Prof. Kitila Mkumbo kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji
Leo asubuhi Rais John Pombe Magufuli amemteua Mshauri wa Chama chetu Prof.
Kitila Mkumbo kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji.
Chama cha ACT
Wazalendo kimepokea kw mikono miwili taarifa juu ya uteuzi wa mshauri wa chama
chetu Kwa sababu imeonyesha kuwa Rais ameona kuwa hata Watanzania walio kwenye
Vyama vya Upinzani wana uwezo, weledi na uzalendo wa kutumikia nchi yetu.
Kwa
nafasi hii ya Ukatibu Mkuu wa Wizara, ndugu Kitila hawezi kuendelea kuwa
Mshauri wa Chama nafasi ambayo inamfanya kuhudhuria vikao vyote vya Chama ikiwemo
Kamati Kuu.
Ndugu Mkumbo ameandika barua ya kujiuzulu nafasi yake ya mshauri wa
Chama na kubaki kuwa mwanachama wa kawaida tu. Nimeipokea barua yake na
kumkubalia Kwa maslahi mapana ya nchi yetu.
ACT
Wazalendo tunamshukuru ndugu Kitila Mkumbo kwa mchango wake katika uongozi wa
Chama chetu kwa wakati wote ambao alikitumikia Chama chetu kama mshauri wa
chama.
Msimamo wa chama chetu ni utumishi wa kizalendo kwa Taifa utokanao na
kila mwananchi, ndio msingi wa kaulimbiu yetu ya ‘Taifa Kwanza, Leo na Kesho’,
hivyo basi tunamtakia kila la kheri ndugu Kitila katika utumishi wake kwa Taifa
letu katika nafasi yake hii mpya.
Wizara Hii ni kubwa na muhimu Sana kwa nchi
yetu. Maji ni tatizo moja kubwa ambalo wananchi wetu wanakumbana nalo na Kama
Taifa hatujaweza kulimaliza.
Tunamtakia kila la kheri ndugu Mkumbo katika
kuongeza nguvu kumaliza kero ya maji na kuhakikisha tunaimarisha Kilimo cha
Umwagiliaji nchi nzima. Tunamsihi aanze na ajenda ya Mfuko wa Maji Vijijini na
kuanzishwa Kwa Wakala wa Maji Vijijini utakaosimamia upatikanaji wa Maji Kwa
wananchi wetu.
Kwa hatua
hii, tunaona Rais ameamua kuunganisha nchi yetu Kwa kufanya kazi na watu wote
bila kuwabagua Kwa itikadi zao za vyama. Watanzania ni wamoja na kauli za
kuwagawa zinaumiza zaidi Taifa kuliko kuliweka pamoja.
Tunaamini kuwa Rais Ana
nia njema katika uteuzi huu na sisi tumempa baraka zote Mwanachama wetu
mwanzilishi wa Chama kwenda kwenye nafasi ya juu zaidi ya utumishi wa umma.
Tunaamini hatamwangusha Rais na muhimu zaidi hatawaangusha Watanzania.
Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Kiongozi wa Chama – ACT Wazalendo
Aprili 4, 2017
Dodoma.
|
No comments:
Post a Comment