Kila la kheri Serengeti Boys katika Mapambano ya Kuwania Ubingwa wa Afrika. - Mwana Wa Makonda

Breaking

Post Top Ad

Wednesday, April 05, 2017

Kila la kheri Serengeti Boys katika Mapambano ya Kuwania Ubingwa wa Afrika.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiagana na wachezaji wa Serengeti Boys mara baada ya kula nao chakula cha jioni Jana April 4, 2017 ambapo aliwaalika kwenye makazi yake Oyster Bay, Dar es Salaam.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja wachezaji wa timu ya Taifa ya Vijana (Serengeti Boys) mara baada ya kula nao chakula cha jioni ambapo aliwaalika kwenye makazi yake Oyster Bay, Dar es Salaam.

Timu ya Taifa ya Tanzania ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 maarufu kama Serengeti Boys, inatarajiwa kusafiri kesho saa 10.45 jioni kwa Ndege ya Shirika la Ndege la Emirates kwenda Morocco kupitia Dubai, Falme za Kiarabu (UAE).

Timu hiyo yenye Wachezaji 23 na Viongozi Wanane watakuwa Uwanja Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu J.K. Nyerere kuanzia saa 7.00 mchana kwani wanatakiwa kuanza kuingia uwanjani saa 7.45 kwani saa tatu baadaye ndipo ndege itakapopaa.

Wanahabari wanaweza kupata mahojiano ya mwisho kadhalika kupata picha za habari wakati huo wa mchana kabla hawajaingia ndani kwenye ukaguzi wa taratibu za (check in logistics).

Kabla ya kusafiri, timu hiyo ilikuwa kambini hapa nyumbani tangu Januari 29, mwaka huu 2017 na baada ya kambi ya mwezi mmoja na nusu, ilicheza mechi tatu za kirafiki za kimataifa.
Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Dk. Harrison Mwakyembe akizungumza wakati wa hafla fupi ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa timu ya Serengeti Boys,jana usiku tarehe 04, Aprili 2017, Oyster Bay jijini Dar es Salaam.

Machi 30, 2017 ilicheza Burundi ‘Intamba Murugamba’ na kushinda mabao 3-0 kabla ya kurudiana tena Aprili 1, mwaka huu na kushinda mabao 2-0. Mechi zote mbili zilifanyika Uwanja wa Kaitaba, ulioko Bukoba mkoani Kagera.

Mechi ya mwisho hapa nyumbani ilifanyika Aprili 3, mwaka huu dhidi Ghana ‘Black Starlets’ na kutoka sare ya 2-2 katika mchezo ulifanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Serengeti Boys ilitumia mchezo kama ishara ya kuwaaga mamilioni ya Watanzania kabla ya kusafiri kwenda kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana zitakazofanyika Gabon kuanzia Mei 14, mwaka huu.
Waziri wa Habari Utalii Utamaduni na Michezo Zanzibar Mhe. Rashid Ali Juma akizungumza wakati wa hafla ya chakula cha jioni kwa timu ya Taifa ya Serengeti Boys iliyoandaliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Serengeti Boys itakuwa Rabat, Morocco kufanya kambi ya takribani mwezi mmoja kuanzia Aprili 5, mwaka huu. Ikiwa huko angalau itacheza mechi za kirafiki zisizopungua mbili dhidi ya wenyeji morocco na timu nyingine ya jirani ama Tunisia au Misri.

Kambi hiyo ya Morocco itamalizika Mei mosi, mwaka hu ambako timu itasafiri hadi Cameroon. Ikiwa Cameroon, timu itacheza mechi mbili za kirafiki za kimataifa dhidi ya wenyeji yaani Mei 3 na 6, mwaka huu kabla ya kusafiri Mei 7, mwaka huu,2017 kwenda Gabon ambako Serengeti Boys imepangwa kundi B pamoja na timu za Mali, Niger na Angola.

Vipimo vya mechi dhidi ya Ghana kadhalika hapo baadaye Cameroon, vitakuwa mwafaka kwenye kufanya tathmini ya uwezo wa Serengeti Boys kwani wapinzani hao wamekuwa na rekodi nzuri kwenye soka la vijana na kwa kipindi hiki zimepangwa kundi A pamoja na wenyeweji Gabon na Guinea.

Nahodha wa timu ya Serengeti Boys akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake mbele Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan (kulia) wakati wa hafla fupi ya kuwatakia heri Serengeti Boys ambao wanajiandaa na fainali ya Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 yanayotarajiwa kufanyika Nchini Gabon.

Kila la kheri Serengeti Boys katika mapambano ya kuwania ubingwa wa Afrika kadhalika kucheza fainali za Kombe la Dunia hapo Novemba, mwaka huu,2017 zitakazofanyika India. 

Serengeti Boys inaweza na Mtanzania tunakuomba kuichangia timu hii kwa namna ya 223344 kupitia mitandao yote ya simu.

Post Bottom Ad