Rais Magufuli azindua uwanja wa Ndegevita wa Ngerengere mkoani Morogoro. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Tuesday, March 07, 2017

Rais Magufuli azindua uwanja wa Ndegevita wa Ngerengere mkoani Morogoro.

Rais na Amiri Jeshi Mkuu Dkt John Pombe Magufuli na Balozi wa China hapa nchini Dkt. Lu Youqing wakifunua kitambaa kuashiria uzinduzi  rasmi ya Uwanja wa kisasa wa ndegevita wa Ngerengere mkoani Morogoro jana Machi 6, 2017.

Rais na Amiri Jeshi Mkuu Dkt John Pombe Magufuli akijiandaa kufyatua risasi ya bastola kuashiria matumizi rasmi ya Uwanja wa kisasa wa ndegevita wa Ngerengere mkoani Morogoro Jana Machi 6, 2017.

Rais na Amiri Jeshi Mkuu Dkt John Pombe Magufuli na Balozi wa China nchini Dkt. Lu Youqing katika picha ya pamoja na viiongozi mbalimbali baada ya uzinduzi  rasmi ya Uwanja wa kisasa wa ndegevita wa  Ngerengere mkoani Morogoro.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, hapo jana tarehe 06 Machi, 2017 amezindua uwanja wa kisasa wa ndegevita wa Ngerengere uliopo Mkoani Morogoro, uliofanyiwa ukarabati mkubwa baada ya miundombinu ya uwanja uliojengwa tangu mwaka 1970 kuharibika.

 Sherehe ya uzinduzi wa uwanja huo imefanyika uwanjani hapo na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Balozi wa China hapa nchini Mhe. Dkt. Lu Youqing, Viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama na Wakuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania wastaafu.

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance Salvatory Mabeyo amesema ukarabati wa uwanja huo ulioanza tarehe 15 Julai, 2013 umegharimu Shilingi Bilioni 137 na Milioni 631 ikiwa ni ufadhili wa Serikali ya China na umehusisha kujenga upya njia ya kuruka na kutua ndege yenye urefu wa mita 3,000 upana wa mita 45 na unene wa sentimeta 45 pamoja na maegesho ya ndege za kivita na ndege za abiria.

Jenerali Mabeyo ameongeza kuwa uwanja huo ni miongoni mwa viwanja bora zaidi duniani kwa sasa na una uwezo wa kutumiwa na ndege za aina zote zilizo chini ya Boeing 777 huku akibainisha kuwa pamoja na ndege za kivita pia unaweza kutumiwa na ndege za kawaida za abiria kwa dharula.

Nae Balozi wa China hapa nchini Mhe. Dkt. Lu Youqing amesema kujengwa kwa uwanja huo kumeimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na China na amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kuendeleza uhusiano huo.

Pamoja na kuzindua uwanja huo, Mhe. Rais Magufuli ameshuhudia maonesho ya ndege za kivita zilizorushwa kwa mbinu mbalimbali za kivita, kutoa heshima na kutua katika uwanja huo.

Katika hotuba yake, Mhe. Rais Magufuli amelipongeza Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kazi kubwa linayofanya na pia amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Xi Jinping na Serikali yake kwa msaada mkubwa iliyoutoa kujenga uwanja huo.

Mhe. Balozi Lu Youqing naomba unipelekee shukrani zangu za dhati Mhe. Rais wa China kwa kutoa msaada huu mkubwa wa kujenga uwanja wa ndegevita wa Ngerengere, najua China imetusaidia kujenga Reli ya TAZARA, Kiwanda cha Urafiki na Uwanja wa Mpira, hii yote inathibitisha uhusiano wetu mzuri, urafiki na undugu” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Aidha, Mhe. Dkt. Magufuli ameahidi kujenga barabara ya lami ya kuunganisha Kamandi ya Jeshi la anga ya Ngerengere na barabara kuu ya Dar es Salaam – Morogoro.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad