Rais Dkt. Magufuli Afuta Agizo la Kufunga Ndoa kwa Sharti la kuwa na Cheti cha Kuzaliwa. - Mwana Wa Makonda

Breaking

Post Top Ad

Friday, March 17, 2017

Rais Dkt. Magufuli Afuta Agizo la Kufunga Ndoa kwa Sharti la kuwa na Cheti cha Kuzaliwa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Wanahabari Mkoani Dodoma kuhusiana na kufuta agizo lililotolewa jana March 16,2017 na Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Harrison Mwakyembe kuhusu Wananchi wanaohitaji kufunga ndoa kuanzia mwezi Mei mwaka huu,2017 kuwa na vyeti vya kuzaliwa. 

Rais Magufuli amefuta agizo hilo leo March 17, 2017 (Ijumaa) wakati akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi kabla ya kuondoka katika Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma na kurejea Jijini Dar es Salaam.

Amesema Serikali haiwezi kuruhusu sharti hilo kutumika kwa kuwa litawanyima haki ya kuoa na kuolewa Watanzania wengi ambao hawana vyeti vya kuzaliwa, huku utaratibu wa kupata vyeti hivyo ukiwa bado unakabiliwa na changamoto nyingi kwa wanaohitaji.

Amesema mpaka sasa idadi ya Watanzania walio na vyeti vya kuzaliwa ni chini ya asilimia 20 huku wengi wao wakiwa ni wananchi waishio vijijini ambako ni vigumu kupata vyeti hivyo, na wengine wakiwa ni waliozaliwa kabla ya kuanza kutolewa kwa vyeti vya kuzaliwa nchini mwaka 1961.


Rais Mhe. Dkt. Magufuli ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kupata vyeti vyao vya kuzaliwa kama kawaida na amewataka viongozi wote kuwahamasisha wananchi kuwa na vyeti hivyo. 

Kushoto Pichani kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bw.Jordan Rugimbana. 

PICHA NA IKULU.

Post Bottom Ad