Kutajwa Orodha ya RC Makonda:Yusuf Manji amwaga mamilioni kwenye ‘Google Ads’ kujisafisha. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Thursday, February 09, 2017

Kutajwa Orodha ya RC Makonda:Yusuf Manji amwaga mamilioni kwenye ‘Google Ads’ kujisafisha.Siku moja baada ya mfanyabiashara maarufu na mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Yusuf Manji kutajwa na mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwenye orodha ya pili ya watu wanaoshukiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya, amemwaga mamilioni ya fedha kulipia matangazo ya mtandaoni, Google Ads kujisafisha.

Matangazo hayo yanaonekana kwenye tovuti nyingi, hata za nje unazozifungua kuanzia Alhamis hii.

Hatua hiyo pia imekuja saa chache baada ya Manji kuitisha mkutano na waandishi wa habari kuzungumzia kutajwa kwake ambako alisema amedhalilishwa na kwamba ataenda polisi Alhamis hii badala ya Ijumaa kama ambavyo Makonda aliwataka.

Matangazo hayo yanaonesha bango lenye picha yake na maelezo yasemayo ‘Yes I ‘am addicted to Yanga.’

Ukiclick, inakupeleka kwenye maelezo marefu yanayomwelezea mfanyabiashara huyo pamoja na mambo aliyoyafanya.

Maelezo hayo ni kama yafuatayo:
Manji Mwenyekiti wa kihistoria Yanga
MWENYEKITI wa klabu ya soka ya Yanga ya Dar es Salaam, Yusuf Mehboob Manji ni mmoja wa matajiri wa hapa nchini ambao ni wapenda mpira wa miguu na wamekuwa tayari kuwekeza utajiri wao kwa asilimia kubwa kwenye mchezo huo. Manji ambaye alisomea uongozi wa biashara katika vyuo vikuu vya Uswisi na Marekani amekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Kampuni ya Quality Group tangu mwaka 1995.
Kampuni hiyo imekuwa ikifanya shughuli nyingi za uzalisha, usambazaji, utengenezaji na uuzaji wa bidhaa mbalimbali ndani na nje ya nchi. Anakadiriwa kuwa na utajiri unaofikia dola milioni 700 ambazo ni zaidi ya shilingi trilioni 1.5 za kitanzania.
Ni Mwenyekiti kijana zaidi kuwahi kutokea ndani ya Yanga, katika uongozi wake hajawahi kuchukuwa posho wala mshahara wa aina yoyote. Mbali na hilo pia Manji hawajawahi kutengeneza faida yoyote akiwa kwenye klabu hiyo yenye maskani yake kwenye mitaa ya Twiga na Jangawani, Ilala, Dar es Salaam.
Yeye kwake kuwekeza mabilioni ya fedha kwaajili ya kuchangia maendeleo ya sokana kuwapa furaha watu wengine wala haoni tabu. Manji ameingia kwenye orodha ya wafadhili wa kukumbukwa zaidi Tanzania ambapo kwenye orodha hiyo wamo pia akina Shiraz Sharif, Ahmed Bora, Shafi Bora, Mohamed Virani, Azim Dewji, Abbas Gulamali, Murtaza Dewji, Mohamed Dewji, Naushad Mohamed na Abdulsasattar.
Ukijarikubu kuvuta kumbukumbu zako kwa miaka ya nyuma zaidi hautaweza kupata mtu ambaye alifanya mambo makubwa zaidi ya anayofanya Manji ndani ya Yanga. Ndani ya Yanga alijijengea heshima kubwa baada ya kumaliza mgogoro mkubwa baina ya makundi ya Yanga Asili na Yanga Kampuni ambao uliokuwa ukiitafutana na kuigawa timu hiyo kwa kipindi kirefu. Mgogoro huo ulizikwa na ikarejeshwa Yanga moja tu, ile inayobeba kaulimbiu, Daima mbele, Nyuma mwiko.
Kinara wa lililokuwa kundi la Yanga Asili, Yussuf Mzimba na yule wa lililokuwa kundi la Yanga Kampuni, Francis Kifukwe walipeana mikono na kuunganisha nguvu zao, kuelekea katika kuisimamisha vizuri. Kitu hicho ndiyo kinachosababisha wana Yanga kutomuelewa mtu yoyote ambaye amekuwa na lengo la kupenyeza figisu kwa namna yoyote ile ndani ya timu hiyo.
Fedha na utajiri wake uliweza kusaidia maendeleo ya mpira wa miguu nchini na hasa kwa klabu ambayo kwa muda mrefu amakuwa na mafungamano nayo ya Yanga. Aliingia Yanga, Juni, mwaka 2006 akiwa kama mfadhili wa klabu ambapo kwa kutumia fedha zake aliweza kukijenga kikosi bora cha timu hiyo katika nyanja mbalimbali.
Alisaidia kwa kiasi kikubwa katika kuhakikisha timu inakuwa katika mandhari nzuri huku wachezaji wakipata kila wanachokitaka kwa wakati. Manji alihakikisha timu ya Yanga inafanya usajili wa wachezaji na makocha wazuri iwe wa ndani au wa nje ya nchi bila kujali gharama ya kuwanunulia na gharama ya mishahara watakayolipwa. Nani asiyekumbuka katika enzi za mwanzo wa ufadhili wa Manji kwa Yanga kwamba kulikuwa na posho hata kwa anayefunga bao mazoezini?
Ama hakika kama kuna jina la watu waliopita ndani ya Yanga na kudumu milele basi jina la Manji halipaswi kusahaulika hata kwa sekunde moja. Kuna msemo wa waswahili huwa unasema kuwa kutoa ni moyo na wala si utajiri na hapa kwa kiasi kikubwa unaweza kuona ni kwa namna gani Manji alikuwa anatoa kutokana na moyo wake kufungamana na mchezo wa soka na wala si kwaajili ya utajiri wake.
Kwani kuna matajiri wangapi ambao wana fedha nyingi nchini nab ado hawakuwa kuthubutu kufanya hata nusu ya mambo ambayo Manji aliwahi kuyafanya na ambayo bado anaendelea kuyafanya ndani ya Yanga. Wengi watakuwa na kumbukumbu ya tukio la kustaajabisha la katikati yam waka jana ambapo Yanga ikiwa kwenye michuano ya Shirikisho ya Afrika.
Kwenye michuano hiyo Yanga walipangwa kwenye kundi A wakiwa na timu za Medema ya Ghana na TP Mazembe ya DR Congo na MO Bejaia ya Algeria. Baada ya Yanga kufungwa bao 1-0 huko Algeria walikuja nyumbani kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kucheza na TP Mazembe na ili kuiongezea nguvu timu yake Manji aliamua kuinunua mechi hiyo na kuingiza mashabiki wote bure.
Hilo lilikuwa ni kama tukio lililoshangaza wengi lakini kwa wanamjua Manji na kwa namna anavyojitolea wanaweza wasishangae sana kwani mwaka 2007, tajiri huyo alimwaga kiasi cha shililingi milioni 200 kwaajili ya kuwaruhusu Watanzania kuingia ndani ya uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza kuwaunga mkono Yanga wakati wanacheza na Al Hilal ya Sudan. Mechi hiyo ilikuwa ni ya Kombe la Shirikisho la Afrika pia na matokeo yake ilikuwa ni 0-0.
Kujitolea kwa Manji kwa Yanga hakuweza kuishia hapo na katu hakukuwahi kufikiriwa kuwa kutakuja kuwa na ukomo kwani amekuwa akifanya mambo makubwa zaidi kila baada ya kufanya jambo moja.
Apewa uchifu na wazee
Tukio hilo linakumbukwa kufanyika baada ya kumaliza utata na mgororo baina ya pande mbili kinzani. Katika kipindi anasuluhisha ugomvi huo alikuwa ni kijana mdogo mwenye umri wa miaka 33 tu na wengi waliona kuwa amefanya mambo makubwa kuliko hata umri wake.
Aliweza kuanzisha bodi ya kwanza wadhamini ndani ya timu hiyo ikiongozwa na kina Francis Kifukwe huku pia akianziha baraza la wazee ambalo linaongozwa na kina Abeid Mzimba na Mzee Akilimali.
Baada ya kazi hiyo kukamilika na kuhakikisha Yanga ipo kwenye utulivu Manji aliomba kukaa pembeni na kuendelea kuwa kama mfadhili kitu ambacho kiliwafanya wazee wa timu hiyo wamtukunuku na kumsimika UCHIFU kwa kumkabidhi nembo ya klabu na mkuki.
Kurudi kuwa Mwenyekiti
Baada ya kukaa kwa muda mrefu kipindi cha takribani miaka 6 akiwa kama mfadhili ndipo ilipotokea nafasi ya viongozi wa Yanga waliochaguliwa na wanachama kuingia katika kashfa mbalimbali. Viongozi hao ambao hawakuwa waaminifu waliweza kubadhilisha fedha za Manji na kufanya baadhi ya shughuli za maendeleo kutofanyika kwa kiwango ambacho kilitarajiwa na mtoa fedha ambaye ni mfadhili wao Manji.
Kutokana na jambo hilo iliepelekea baadhi ya matokeo ndani ya timu kuwa mabaya kufikia hatua ya kufungwa mabao 5-0 na wapinzani wao wa jadi Simba.
Suala hilo liliwafanya wanachama wa Yanga kuwashinikiza viongozi hao mwaka 2012 kujiuzulu mara moja kitu ambacho kilitekelezeka na wengi baada ya hapo walipendekeza Manji mwenyewe ndiyo agombee kwenye uchaguzi ili kuanza kuiongoza Yanga.
Kwenye uchaguzi ambao ulikuwa wa kidemokrasia uliofanyika siku ya Jumapili Julai 14, 2012, Manji akiwa na umri wa miaka 36 tu aliweza kushinda kwa kishindo akiibuka na ushindi wa asilimilia 97.5.
Ulikuwa wakidemokrasia kwasababu kila mmoja aliruhusiwa kuchukuwa fomu n ahata kumpa upinzani Manji na waliibukaJohn Jembele aliyepata kura 40(2.6%) na Edgar Chibura aliyepata kura 4(0.24%) dhidi ya kura 1876(97.0%) ambazo Manji alipata.
Katika uchaguzi wa awamu ya pili ambao ulifanyika Juni mwaka jana, Manji alipita bila kupingwa huku Makamu wake Clement Sanga akishinda kwa kishindo.
Mambo makubwa aliyoifanyika timu
Ikiwa chini ya Manji, Yanga iliweza kuonesha utawala wake na ufahari ndani nan je ya nchi huku timu hiyo ikianza kupewa majina mengi ya utani kama vile matajiri wa nchi na wakimataifa katika hali ya kusadifu maisha yao bora chini ya mwenyekiti wao.
Yanga iliweza kufanya mambo mengi ambayo kwa timu nyingine yatabaki kuwa ndoto tu, mara kadhaa timu hiyo imekuwa ikiweka kambi zake za maandalizi kwenye bara la Ulaya na kufikia kwenye hoteli za nyota tano kwa gharama ya Manji.
Zaidi ya mara mbili timu hiyo imeshaweka kambi kwenye nchi ya Uturuki kwaajili ya kujiandaa na mechi zake kadhaa ikiwemo ile ya mara ya mwisho wakati wanajiandaa na TP Mazembe.
Ukiachana na hapo Manji pia amekuwa akitoa fungu kubwa la bajeti kwaajili ya usajili wa wachezaji nyota wakimataifa wakiwemo wa hivi sasa kama vile Donald Ngoma, Obrey Chirwa, Thaban Kamusoko, Haruna Niyonzima. Wengine ni Justine Zullu, Amis Tambwe, Vicent Bosou pamoja na makocha Hans van Pluijm na George Lwandamina
Mafanikio ya Yanga chini ya Manji
Tangu kuanza kwa uongozi wake ndani ya Yanga timu hiyo imekuwa katika hali nzuri ya kimaisha na kuwa bora zaidi kiushindani ndani ya uwanja.
Kwa uongozi madhubuti wa Manji akiwa kama mwenyekiti tangu mwaka 2012 hadi kufikia leo, timu hiyo imefanikiwa kushinda mataji matatu ya ligi kuu (2013, 2015 na 2016) huku wakiwa kwenye nafasi nzuri ya kushinda taji la msimu huu. Mbali na mataji hayo pia Yanga chini ya uongozi wa Manji iliweza kutwa mataji mawili ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashiriki na Kati (Kagame) katika miaka ya 2011 na 2012.
Pia Yanga kwa mara ya kwanza baada ya miaka 18 ilifanikia kutinga hatua ya nane bora (robo fainali) ya michuano ya Kombe la Shirikiho la Afrika. Yanga pia ilishinda kombe la FA mwaka 2016 na mataji matatu ya ngao ya jamii.
Pia tangu Manji alipoanza kuiongoza Yanga, timu hiyo imekutanana watani zao Simba kwenye michezo ya ligi kuu bara mara tisa ambapo Yanga wameshinda mara tatu wakifungwa mchezo mmoja na kwenda sare mara tano. Mwenyewe anasema kuwa mafanikio ya Yanga yamemfanya kuwa na heshima kubwa nchini miongoni mwa mashabiki na kwa wananchama.
Yeye na familia yake amekuwa katika hali ya kujihisi ni kama mfalem pindi anapokatiza katika maeneo mbalimbali na watu kujua kama ni yeye.
Mke, watoto na hata watoto wake wamekuwa wakionekana kama wafalme na malkia pindi wanapokuwa kwenye matembezi yao na imefakia hatua ya hata kupewa bidhaa bure wanapotembelea kwenye baadhi ya maduka mara tu baada ya kugundulika kuwa wanatoka kwenye familia ya Manji. “Kwa mapenzi haya ninayoyapata nina ahidi kuwa nitaendelea kufanya kila niwezalo kwa uwezo wangu wote kwa hali na mali katika kipindi changu chote ambacho nitakuwa mwenyekiti wa Yanga kuhakikisha kuwa timu inakuwa imara zaidi,” alisema Manji.

Post Bottom Ad