Shughuli za Kilimo, Ufugaji na Makazi Zauharibu Msitu wa Biharamulo – Kahama. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Thursday, October 20, 2016

Shughuli za Kilimo, Ufugaji na Makazi Zauharibu Msitu wa Biharamulo – Kahama.

Hizi ni miongoni mwa athari za uvamizi wa wananchi hao katika Hifadhi ya Misitu wa Biharamulo - Kahama Wilayani Chato Mkoa wa Geita ambapo miti ya asili imekatwa kupisha shughuli za kilimo, ufugaji na makazi bila kujali athari za tabianchi.

Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani akionesha moja ya kigingi (beacon) cha mpaka wa Hifadhi ya Msitu wa Biharamulo - Kahama uliopo Wilayani Chato Mkoa wa Geita ambao umevunjwa na wananchi waliovamia msitu huo kwa ajili ya kuendesha shughuli za kilimo, ufugaji na makazi. Wa pili kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Geita, Meja Gen. Mstaafu Ezekiel Kyunga na Mkuu wa Wilaya ya Chato, Shaaban Ntarambe (kulia).
Na Hamza Temba - WMU
___________________________________________________________

Wananchi wanaozunguka hifadhi za misitu na wanyamapori nchini wametakiwa kutii sheria za uhifadhi na kujiepusha na vitendo viovu vya uharibifu wa mazingira vinavyopelekea kupotea kwa uoto wa asili na kutishia nchi kuwa jangwa ambapo pamoja na mambo mengine wametakiwa kuondoa mifugo yao katika maeneo yaliyohifadhiwa kisheria.

Hayo yamesemwa Oktoba 18,2016, Mkoani Geita na Naibu Waziri, Wizara ya Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani wakati akizungumza na viongozi na watendaji wa Mkoa huo Wilayani Chato kuhusu maelekezo ya kuwaondoa wananchi waliovamia maeneo hifadhi Mkoani humo na taifa kwa ujumla.

Alieleza kuwa vitendo hivyo vya uharibifu wa mazingira ni pamoja na ukataji wa miti hovyo, kilimo kisichoendelevu, uchungaji holela wa mifugo, uanzishaji makazi na shughuli zingine za kibinadamu katika maeneo yaliyohifadhiwa kisheria ikiwemo Hifadhi za Misitu, Mapori ya Akiba, Mapori Tengefu na Hifadhi za Taifa.

"kwa sasa Tanzania inapoteza takriban hekta 372,000 za uoto wa asili kila mwaka na endapo hali hiyo ikiachwa iendelee tishio la kutoweka kwa uoto huo ni kubwa zaidi. Takwimu pia zinaonyesha kuwa Tanzania ina eneo la uoto wa asili lenye ukubwa wa takriban Hekta milioni 48.1 na kwamba kasi hiyo ikiachwa iendelee itaiacha Tanzania bila uoto wa asili baada ya miaka 129" alisema Makani.

Akizungumzia taratibu za kuwaondoa wananchi katika maeneo yaliyohifadhiwa kisheria alisema watumishi na viongozi wote wa Serikali wanaotekeleza zoezi hilo wanatakiwa kufuata sheria na miongozo iliyowekwa ikiwa ni pamoja na kujiepusha na vitendo viovu vinavyoweza kuichafua Serikali ikiwemo rushwa na unyanyasaji wa wananchi, "watakaobainika kwenda kinyume na utaratibu huo watachukuliwa hatua za kisheria" alisema.

Katika utekelezaji na usimamizi wa sheria hizo za uhifadhi, aliwataka watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii kusimamia sheria hizo kila siku na kuendesha utekelezaji wake kwa kushirikiana na kamati za ulinzi na usalama za Wilaya na Mikoa ili kuimarisha utekelezaji wa sheria hizo na kuweka uwazi katika utendaji.

Kwa upande wa wananchi ambao wapo katika vijiji na vitongoji vilivyosajiliwa kisheria aliwataka kutoanzisha au kuendeleza shughuli mpya za kibinadamu hususani zinazosababisha uharibifu wa mazingira ikiwemo kuathiri mabadiliko ya tabia nchi mpaka pale kikosi kazi cha kitaifa kitakapokamilisha kazi yake na kuishauri Serikali namna bora ya kumaliza migogoro ya ardhi nchini.

Maagizo hayo yamekuja ikiwa ni siku chache kabla ya kikosi kazi hicho ambacho kimeundwa na Serikali kikiwa na wajumbe kutoka Wizara sita zinazohusika moja kwa moja na changamoto mbalimbali za ardhi kwa madhumuni ya kufanya uchunguzi wa kina ikiwemo kupitia sheria zote zinazohusika kabla ya kuishauri serikali namna bora ya kumaliza migogoro ya ardhi ikiwemo kwenye maeneo ya hifadhi.

Makani alizitaja wizara hizo kuwa ni Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Maliasili na Utalii, TAMISEMI na Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambazo ndizo zimeanza utekelezaji wa zoezi hilo linalotarajiwa kukamilika mwezi Desemba mwaka huu. 

Alisema Wizara nyingine mbili zitaungana baadae kukamilisha zoezi hilo ambazo ni Maji na Umwagiliaji na Nishati na Madini.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita, Meja Gen. Mstaafu Ezekiel Kyunga alisema Mkoa wake unakabiliwa na uhaba wa ardhi uliosababishwa na ongezeko kubwa la watu waliovutiwa na shughuli za kiuchumi Mkoani humo ikiwemo uchimbaji wa madini, uvuvi, ufugaji pamoja na kilimo ambazo kwa namna moja ama nyingine imekuwa ni changamoto kubwa katika uhifadhi Mkoani humo. 

Alieleza changamoto nyingine kuwa ni mitazamo tofauti ya baadhi ya wanasiasa kuhusu uhifadhi.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Chato, Bw.Shaaban Ntarambe alisema kumekuwepo na uharibifu mkubwa wa misitu Wilayani humo ambapo Hifadhi ya Msitu wa Biharamulo - Kahama kwa upande wa Wilaya yake umeharibiwa kwa asilimia 70 kutokana na shughuli za kilimo, ufugaji, uchimbaji madini na makazi ya kudumu hali inayohatarisha kutoweka kwa hifadhi hiyo.

Msitu wa Biharamulo - Kahama una ukubwa wa hekta 134,684 na upo katika Wilaya tatu za Chato, Bukombe na Biharamulo. Kwa upande wa Wilaya ya Chato ambapo uharibifu  huo umefanyika kwa asilimia 70 una ukubwa wa hekta 30,000. 



No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad