Mkuu wa Mkoa wa Kagera Atumbua Jipu Watumishi Wanane wa Halmashauri Bukoba na Ngara kwa Ubadhirifu wa Fedha za Serikali. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Saturday, August 27, 2016

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Atumbua Jipu Watumishi Wanane wa Halmashauri Bukoba na Ngara kwa Ubadhirifu wa Fedha za Serikali.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Meja Jenerali Salum M.Kijuu katika kuteleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alilolitoa tarehe 29/04/2009 linalomtaka kuzisimamia Halmashauri za Wilaya kila moja kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali baada ya kupokelewa kwa taarifa hiyo, Mkuu wa Mkoa  tayari ameagiza kuchukuliwa hatua kwa watendaji 8 waliohusika na uzembe na upotevu wa fedha za Serikali katika Halmashauri mbili za Wilaya alizopitia kusimamia zoezi hilo.

Mhe. Kijuu tayari amesimamia zoezi la kujadili Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali katika Halmashauri za Wilaya ya Bukoba Muleba na Ngara ambapo katika zoezi hilo  aliagiza hatua kuchukuliwa mara moja kwa Watendaji saba Katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba na Mtendaji mmoja katika Halmashauri ya Wilaya ya Ngara.

Katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizoishia tarehe 30 Juni, 2015 ilibainisha hoja zenye tafsiri ya kuwepo Ubadhirifu, wizi na Uzembe pamoja na ukiukaji wa makusudi wa sheria za fedha na sheria za manunuzi ambapo watumishi wafuatao walihusika nao ni kama ifuatavyo:-

Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi (Bi Grace Uyabange), Mfamasia wa Halmashauri (Bw. Edward Kabandami), Mganga Mkuu wa Wilaya aliyehamia Katika Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba (Dk. Hamza Mgula) ambapo Katibu Tawala wa Mkoa aliagizwa Kumrejesha kujibu Hoja zinazomkabiri. 

Wengine ni Afisa Elimu Sekondari (Bw. Lucas Mzungu), Afisa Utumishi (Bw. Maginga Mang’oa), Mhasibu Mapato ya Ndani (Bw. Aristides Rwegoshora) na Mweka Hazina (Bw. Jonathan Katunzi).
Watumishi waliotajwa walihusika kufanya yafuatayo kila mmoja kulingana na nafasi aliyokuwepo kama msimamizi mkuu wa eneo hilo, Kwanza ni kufanya  Mabadiliko ya mkataba wa Ujenzi wa kituo cha Mabasi (Bus Stand) ya Kemondo (Tshs 44 milion) bila idhini ya Bodi ya zabuni ya Halmashauri  kinyume na Kanuni za Manunuzi  kanuni ya 110 (5).

Pili, kulipa Mishahara kiasi cha Tshs 28,072,549/=  iliyolipwa kwa Watumishi hewa (watoro na waliostaafu ) wakiwemo watumishi  wa idara ya Elimu Sekondari ambapo, kutokana na uzembe wa Afisa Elimu Sekondari Wilaya na Afisa Utumishi wa Wilaya (2014/2015) kushindwa kutekeleza majukumu yao ya kukagua na kuchukua hatua za kuwaondoa watumishi wasiostahili kulipwa kwa wakati  katika orodha ya malipo (Payroll), walisababisha Serikali kupata hasara ya Tshs 28,072,549/= na kuzilipa taasisi mbalimbali za fedha makato hewa ya kisheria kiasi cha Tshs 9,811,947.55

Tatu, Kubadili matumizi ya fedha za ujenzi wa daraja la Kyamabale kiasi cha Tshs 200,000,000/= bila kuzingatiwa taratibu za kubadili matumizi ya fedha za maendeleo na kusababisha kutokamilika hadi sasa, ujenzi wa daraja lililolengwa kuondoa kero kwa wananchi halijakamilika na lilitakiwa kukamilika tarehe 26 Oktoba, 2015. 

Nne, Manunuzi ya vifaa tiba na madawa ya Hospitali Tshs 16,339,050/= kufanyika  bila dihini ya Bodi ya zabuni 2009/2010. Hoja hiyo ilitokana na baadhi ya watumishi kutoheshimu sheria na miongozo ya Serikali kwa kisingizio cha dharura.

Tano, Manunuzi ya mafuta ya thamani ya Tshs 12,789,364 (mwaka 2013/14) ambayo kwa sasa ni sawa na lita 6,394 ambayo yangewezesha gari moja kusafiri umbali wa kilometa 31,973. Mafuta hayo pamoja na kulipiwa na Halmashauri, hakuna uthibitisho kuwa yalipokelewa katika vitabu vya kupokea mali za Halmashauri na hakuna udhitisho wa matumizi yake

Haya ni manunuzi hewa.

Sita, Kesi za mapato ya Halmashauri zilizokwishatolewa maamuzi na Mahakama na ilipaswa kutekeleza hukumu kupitia Mwanasheria wa Halmashauri. Zaidi ya Tshs 14,800,000/= za Halmashauri hazijafuatiliwa kwa kutekelezwa ama kukaza hukumu na mwanasheria wa Halmashauri. Saba, Matumizi ya Tshs 7,150,000/= za mapato ya ndani bila kufuata taratibu za fedha na hakuna nyaraka zozote zilizoidhinisha  na kuthibitisha matumizi ya fedha hizi ambazo zilipokelewa na mtunza fedha.

Mwisho, Ujenzi wa ofisi ya Afisa Elimu (Sekondari) Tshs 59,500,000/=. Ofisi hii imekamilika lakini haitumiki  kwa sababu fedha zote zilitolewa na Serikali  lakini Mkandarasi hajalipwa. Hii inaongeza deni la Halmashauri kwa mujibu wa mikataba kwa sababu fedha zilibadilishwa matumizi bila idhini ya Mamlaka.

Kutokana na ukiukaji wa sheria za usimamizi wa watumishi, udhaifu katika usimamizi wa fedha na manunuzi, Mkurugenzi na Baraza la Madiwani wachukue hatua za kinidhamu mara moja na kuniletea taarifa ya utekelezaji wa agizo langu ifikapo tarehe 30 Agosti, 2016.” Aliagiza Mhe. Kijuu.
HALMASHAURI YA WILAYA YA NGARA.

Mhe. Kijuu alimwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ngara Bw. Aidan J. Bahama na Baraza la Madiwani kuchumchukulia hatua za kinidhamu Afisa Manunuzi wa Halmashauri Bi Perpetua Rulimbike ikiwa ni pamoja na kumuondoa katika kitengo cha manunuzi kwa kusababisha upotevu wa Shilingi Milioni 24,000,000/= za mafuta na shilingi milioni 122,000,000/= zisizokuwa na stakabadhi za EFD.

Aidha , Mkuu wa Mkoa aliagiza kuchukuliwa hatua za kinidhamu  ikiwa ni pamoja kusimamishwa kazi kwa Watumishi au Watendaji wa Halmashauri hiyo waliosababisha upotevu wa vitabu vya makusanyo ya mapato ya ndani na kutoa taarifa katika ofisi yake ifikapo tarehe 30, Agosti, 2016

Katika Halmashauri ya Wilaya ya Muleba hakuna Mtumishi aliyechukuliwa hatua.

MAAGIZO MENGINE.

Mkuu wa Mkoa Mhe. Kijuu aliawaagiza Madiwani wa Halmashauri za Wilaya za Bukoba, Muleba na Ngara kutojihusisha na kuchukua tenda au kufanya kazi za Halmashauri zao ili kuondoa maslahi binafsi na Halmashauri zao. 

Pili, Wakurugenzi Watendaji wote kuhakikisha wanafanya manunuzi yote kwa kwa wazabuni wenye  stakabadhi za kielektroniki (EFD).   

Mwisho makusanyo yote ya mapato ya ndani ya Halmashauri husika kukusanywa kwa kutumia mifumo ya  kielektroniki.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad