Halmashauri ya Missenyi , Bukoba na Ngara zaongoza kwa Data Chafu mkoani Kagera. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Thursday, August 25, 2016

Halmashauri ya Missenyi , Bukoba na Ngara zaongoza kwa Data Chafu mkoani Kagera.


Waziri wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angella Kairuki akiwa Mkoani Kagera aliawaagiza viongozi wa Mkoa kuhakikisha wanaondoa data chafu za Watumishi katika mfumo wa utumishi ili kuondokana tatizo la Watumishi hewa.

Mhe. Kairuki alitoa agizo hilo alipokuwa akiongea na Mkuu wa Mkoa Meja Jenarali Mstaafu Salum M. Kijuu ofisini kwake mara baada ya kuwasili Mkoani hapa kwaajili ya kikao kazi cha kuongea na Watumishi wa Serikali kutoka katika Taasisi na Idara mbalimbali za Serikali Mkoani Kagera.

“Mhe. Mkuu wa Mkoa katika Mkoa wako kuna data chafu kama ifuatavyo, katika Sekretarieti ya Mkoa zipo data chafu 21, Bukoba Manispaa 70, Biharamulo 296, Halmashauri ya Wilaya Bukoba 429, Karagwe 211, Muleba 51, Ngara 454, Missenyi 1,608 na Kyerwa 234.”

 Mhe. Kairuki alitoa takwimu hizo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera na kusistiza data hizo kuondolewa katika mfumo mara moja.



Aidha Mhe. Kairuki alifafanua kuwa data hizo chafu zilibainika wakati Wizara yake ikifanya uhakiki wa Watumishi kujiridhisha na takwimu zilizotolewa kuhusu watumishi hewa na kubaini kuwa kuna data chafu ambazo zinasababishwa na baadhi ya Watumishi kutokuwa na akaunti za benki za kupitishia mishahra yao.

Pia baadhi ya nyaraka za Watumishi kutofautiana majina na majina halisi wanayoyatumia kazini na yaliyopo katika mfumo wa Taarifa za kiutumishi na mishahara (HCMIS). 

Vilevile baadhi ya Watumishi kuonekana kuwa tayari wamezidi umri wa miaka 60 ya kustaafu kwa lazima lakini bado wanaonekana kuwa bado wapo kazini na wanalipwa mishara ya Serikali.

Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Kijuu (Pichani Kulia) akitoa taarifa ya Mkoa kwa Mhe. Kairuki alisema kuwa Mkoa wa Kagera una Watumishi 19, 982 aidha, katika zoezi la kuhakiki Watumishi hewa Mkoa ulibaini watumishi hewa 274 waliolipwa kiasi cha shilingi bilioni 1,153,690,895.63 na fedha zilizorejeshwa ni shilingi Milioni 103, 725,731.23 sawa na asilimia 8.8%

Vile vile Mhe. Kijuu alimweleza Waziri Kairuki kuwa Mkoa unakabiliwa na tatizo la baadhi ya nafasi za watendaji kukaimiwa ambapo nafasi hizo ni 59, Jambo ambalo linasababisha baadhi ya maamuzi katika ngazi mbalimbali kutotolewa kwa wakati na kwa usahihi kutokana na Makaimu hao kutokuwa na madara kamili.

Akitoa ufafanuzi Mhe. Kairuki alisema kuwa uhakiki ni zoezi endelevu na kazi hiyo itafanyika kwa kuangalia alama za vidole ili kubaini wale wanaotumia vyeti vya watu wengine na kusisitiza hakuna Mtumishi atakayeonewa katika zoezi hilo.

Alisema pamoja na hilo uhakiki utafanyika kwa kuangalia taarifa mbalimbali za kiutumishi, ikiwamo waliobadili majina endapo kama taratibu za kisheria zilifuatwa ili kubaini waliofanya hivyo kwa nia ovu.

Waziri Kairuki aliainisha kuwa Watumishi wanaokaimu nafasi mbalimbali waangaliwe kama wana sifa zinazostahili ili kubaini wale waliopo na wenye sifa lakini hawajapewa.

Aliwaelekeza Maafisa Utumishi kujielimisha kuhusu Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma ili kuepuka malalamiko miongoni mwa Watumishi na kusema ofisi yake inaandaa mfumo ambao Watumishi wa Umma nchini watawasilisha malalamiko yao kwake pale ambapo hawataridhika na huduma wanazopewa kwa waajiri wao.

Mwisho Mhe. Kairuki alitumia muda mwingi katika kikao kazi na Watumishi kusikiliza kero mbalimbali na masuala mbalimbali yahusuyo watumishi na kuyatafutia ufumbuzi hapo kwa papo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad