RAIS DKT MAGUFULI:-awasihi watanzania kudumisha Amani, Umoja na Utulivu asisitiza Serikali kuhamia Dodoma. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Monday, July 25, 2016

RAIS DKT MAGUFULI:-awasihi watanzania kudumisha Amani, Umoja na Utulivu asisitiza Serikali kuhamia Dodoma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewasihi watanzania kuwaenzi Mashujaa kwa kudumisha Amani, Umoja na Utulivu uliojengwa na mashujaa hao.

Rais Magufuli ametoa rai hiyo leo tarehe 25 Julai, 2016 wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu ya siku ya Mashujaa, yaliyofanyika katika uwanja wa Mashujaa Mjini Dodoma.

Pamoja na kutoa rai hiyo Rais Magufuli ameahidi kuwa atahakikisha azma ya Serikali kuhamia Dodoma inatekelezwa kabla ya kuisha kwa kipindi chake cha uongozi wa miaka mitano.

"Tunapoadhimisha siku ya Mashujaa hatuwezi kumsahau Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Baba wa Taifa alisema makao makuu yawe Dodoma, haiwezekani sisi watoto wake, sisi wajukuu wake tupinge kauli ya Mzee huyu.
"Kwa hiyo nilikwishazungumza na leo narudia hili katika siku ya Mashujaa, mlinichagua ndugu zangu wa Dodoma kwa kipindi cha miaka mitano, hadi sasa miezi minane imepita, nimebakiza miaka minne na miezi minne, nataka kuwathibitishia kuwa katika kipindi cha miaka minne na miezi minne iliyobaki nitahakikisha serikali yangu pamoja na mimi tunahamia Dodoma bila kukosa" Amesema Rais Magufuli.

Kufuatia maelekezo hayo ya Mhe. Rais, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ameagiza Mawaziri wote waanze mara moja kuhamia Dodoma na kwamba yeye mwenyewe atakuwa amehamia Dodoma ifikapo mwezi Septemba mwaka huu,2016.
Amiri Jeshi Mkuu Rais Dkt John Pombe Magufuli akiweka Ngao katika Mnara wa kumbukumbu ya Mashujaa alipoongoza Madhimisho ya Siku ya Mashujaa mjini Dodoma leo Julai 25, 2016 .

Viongozi wengine waliohudhuria maadhimisho hayo ni Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais Mstaafu wa awamu ya Pili Alhaji Ali Hassan Mwinyi, Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson, Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Zubeir Ali Maulid, Mawaziri Wakuu wastaafu Mhe. John Samwel Malecela na Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda, Mabalozi na wanadiplomasia kutoka nchi mbalimbali, Viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama, Viongozi wa vyama vya siasa na dini, maafisa na askari waliopigana vita mbalimbali.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dodoma
25 Julai, 2016.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad