Rais John
Pombe Magufuli jana,february 13,2016, alitumia dakika 55 kuzungumza na wazee wa Dar es Salaam, akigusa
kila sekta wakati akizungumzia mambo aliyoyafanya katika siku 100 na
anayotarajia kufanya.
Katika
hotuba hiyo ambayo aliendelea kuzungumzia jinsi nchi inavyotafunwa, kiongozi
huyo wa Serikali ya Awamu ya Tano aliweka msimamo wake kuhusu mgogoro wa
kisiasa Zanzibar, akisema hataingilia.
Pia
alidokeza kuhusu uteuzi wa wakuu wa mikoa na wilaya, akimhakikishia Mkuu wa
Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda kuendelea au kupandishwa cheo.
Mambo
mengine aliyozungumzia ni mafanikio na changamoto ya elimu bure, ujenzi wa
barabara na madaraja, utendaji wa mawaziri, miradi ya umeme, huduma kwenye
Hospitali ya Muhimbili, vyombo vya habari, na kuwataka wananchi wajitathmini
wamefanya nini katika siku 100 za kwanza za utawala wake.
Dk Magufuli
aliyekuwa ameambatana na Makamu wa Rais, Samia Suluhu, Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa, Naibu Spika Dk Tulia Ackson, alikuwa akizungumza na baraza la wazee
wa Dar es Salaam kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, ikiwa ni siku yake ya 102
tangu alipoapishwa Novemba 5, 2015 kuwa Rais.
Mkutano huo
ulihudhuriwa na watu zaidi 3,000, wakiwamo mawaziri, viongozi wa CCM na
viongozi wa dini, walioongozwa na Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaj Mussa
Salum na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.
Rais
Magufuli aliyeingia katika ukumbi huo saa 8:30 mchana, alianza kuzungumza saa
9:36 alasiri na kumaliza saa 10:32 jioni, akisisitiza wananchi wamuombee aweze
kutekeleza majukumu yake, ikiwa ni pamoja na kutumbua majipu.
Uchaguzi Zanzibar
Rais ambaye
amekuwa kimya kwa muda mrefu kuhusu mgogoro wa kisiasa Zanzibar, hatimaye jana
aliweka bayana msimamo wake akisema hataingilia kwa kuwa anaheshimu utawala wa
sheria.
“Tume ya
Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ni huru kwa mujibu wa Kat iba ya Zanzibar kifungu
kati ya 112 au 115. Lakini kama ilivyo kawaida Tume huru ya uchaguzi duniani
haiwezi kuingiliwa na rais yoyote. Ni kama ilivyo ZEC na (Tume ya Taifa ya
Uchaguzi) NEC ndivyo ilivyo,” alisema Rais.
Alisema
uamuzi wa ZEC kufuta uchaguzi Zanzibar na kisha kutangaza tarehe ya marudio,
hauwezi kuingiliwa na mtu yeyote, akisisitiza kuwa wanaotaka tafsiri ya
kisheria juu ya uamuzi wa ZEC, waende mahakamani.
“Mahakama
ipo hutaki kwenda halafu unasema Magufuli ingilia! Nenda mahakamani ukapewe
tafsiri ya haki. Siingilii na nitaendelea kukaa kimya. Jukumu langu ni
kuhakikisha usalama wa Zanzibar, Pemba na Tanzania unaimarika,” alisema.
“Ukifanya
“fyokofyoko” katika eneo lolote nchini, utashughulikiwa na vyombo vya ulinzi na
usalama.”
Mgogoro wa
kisiasa Zanzibar uliibuka baada ya ZEC kufuta matokeo ya uchaguzi wa rais,
wawakilishi na madiwani kwa maelezo kuwa sheria na kanuni zilikiukwa na baadaye
kutangaza Machi 20 kuwa siku ya kupiga kura upya.
Wakati
mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha akitangaza kufuta matokeo siku ambayo
alitakiwa amtangaze mshindi wa kiti cha urais, tayari matokeo ya majimbo 31
yalikuwa yameshatangazwa huku majimbo tisa yakiwa yameshahakikiwa. Pia washindi
wa viti vya uwakilishi na udiwani walishatangazwa na kupewe hati za ushindi.
Chama kikuu
cha upinzani Zanzibar, kimepinga ZEC kufuta matokeo kikisema ni kukiuka katiba
kwa kuwa ushindi unapingwa mahakamani tu na kimejitoa kwenye uchaguzi wa
marudio huku kikimtaka Rais Magufuli aingilie katika kutatua mgogoro huo
mezani.
“Sitaingia
suala la Zanzibar,” alisema Magufuli.
Akizungumzia
mabadiliko ambayo Serikali yake inayafanya, Rais alisema yana changamoto zake
ambazo zinaweza kuwagusa baadhi ya watu, lakini akasema watakaoguswa ni
wachache kwa faida ya wengi.
“Tanzania
haitakiwi kuwa na wanafunzi wanaokaa chini, watu kukosa maji, Muhimbili watu
kulala watano kitandani. Tanzania hii ina neema ila lazima tutambue wapo watu
wachache waliotufikisha hapa,” alisema.
Alisema
mabilioni ya fedha za Watanzania yanatumika hovyo.
“Ifike
mahali Watanzania tujiulize tumemkosea nini Mungu? kwa nini asitusamehe kwa
makosa tuliyoyafanya. Serikali imejitoa sadaka kwa ajili ya Watanzania,”
alisema.
“Ndani ya
Serikali tumejipanga, anayetaka kutukwamisha tutambomoa kwa faida ya
Watanzania, hasa wanyonge. Haiwezekani kila mahali unapokwenda ukute wananchi
wanalia wakati nchi ina rasilimali za kila aina.”
Ufisadi.
Katika
hotuba yake ambayo mara kwa mara alikuwa ikikatishwa na shangwe za wananchi, Dk
Magufuli alianza kuzungumzia ufisadi, akisema katika siku 100 ambazo amekaa
madarakani, wamejifunza mengi na kukumbana na changamoto lukuki.
“Wapo watu
katika nchi hii kwao fedha sio tatizo, fedha hizo hawajazipata kwa uhalali
wamezipata kutoka kwa masikini wanaohangaika . Kila tulipokuwa tunagusa kuna
maajabu,” alisema
Alisema
alimtuma Majaliwa kwenda bandarini na Katibu Mkuu wa Tamisemi kwenda wilayani
Bariadi na wakakumbana na madudu.
“Akiwa
Bariadi alikuta barabara ya kilomita moja imejengwa kwa Sh2 bilioni tena ni
barabara ya halmashauri ya wilaya. Mimi nimekaa Serikalini sijawahi kujenga
barabara kuu ya kilomita moja kwa Sh2 bilioni, ila hii ya halmashauri imejengwa
kwa kiasi hicho?” alihoji.
“Barabara ya
kilomita nne na nusu ya Halmashauri ya Bariadi imejengwa kwa Sh9.2 bilioni,
wakati mkuu wa mkoa, wilaya, mkurugenzi na mhandisi yupo.
“Ninapozungumza kutumbua majibu, Watanzania
mtuunge mkono tuyatumbue kwelikweli.”
Alisema
kiwango hicho cha fedha kingeweza kutengeneza kilomita 22 hadi 23 za lami.
Wizi
bandarini.
Akizungumzia
wizi wa mafuta bandarini alieleza kushangazwa na kitendo cha mita za mafuta
kutofanya kazi kwa miaka mitano.
“Waziri Mkuu
alikwenda bandarini na kukuta flow meter ya kupimia mafuta yanayoingia nchini
haifanyi kazi kwa miaka mitano,” alisema.
“Mafuta
yanaingia nchini yanagawiwa kwa watu na ndiyo maana mnaona kutoka Dar es Salaam
kwenda Kibaha kila mahali kuna sheli (vituo vya mafuta).”
Kutokana na
wizi huo wa mafuta, juzi Majaliwa alimsimamisha kazi mtendaji mkuu wa Wakala wa
Vipimo (WMA) na meneja wake wa kitengo cha bandari kupisha uchunguzi.
Alisema
fedha ambazo zingepatikana kama mafuta hayo yangepimwa na kulipiwa kodi
zingeweza kutumika kununua dawa hospitali, kusomesha wanafunzi bure na kujenga
barabara.
“ Hiyo ndiyo
Tanzania tuliyoikuta sisi. Mifano ni mingi ya kila aina,”alisema.
Madudu
muhimbili.
Alisema
alitembelea Muhimbili na kusimamishwa na akinamama waliomtaka aende wodi ya
wanawake, lakini wasaidizi wake wakamzuia.
“Walinizuia
ila nilikataa. Niliwambia naenda hukohuko na niliyoyakuta ni maajabu,” alisema.
Alisema
katika wodi namba 36, alikuta maji kutoka chooni yanavuja huku akina mama
wakiwa wamelala chini, watano kwenye godoro moja.
“Ukiwa
unaenda Muhimbili jirani kuna jengo la ghorofa tatu, linatumika kama ofisi ya
uzazi na watoto. kuna wafanyakazi 70. Ukisogea mbele zaidi kuna jengo lilianza
kujengwa tangu utawala wa Serikali ya Awamu ya Pili mpaka leo halijaisha,”
alisema.
“(Rais wa
Serikali ya Awamu ya Pili, Ali Hassan) Mwinyi hakulimaliza, akaja (wa Awamu ya
Tatu, Benjamin) Mkapa hakulimaliza, akaja (wa Awamu ya Nne, Jakaya) Kikwete
hakulimaliza na sasa nipo mimi bado halijaisha.”
Alisema
inashangaza kuona viongozi wa hospitali hiyo wakishindwa kumfukuza mkandarasi
anayejenga jengo hilo ambaye ni Masasi Construction Engineering .
Alisema
alipokuwa Waziri wa Ujenzi alifukuza makandarasi 3,000, lakini akashangazwa
kuona jengo la ghorofa nne likijengwa zaidi ya miaka 20.
“Nadhani
jengo hili limeweka rekodi duniani,” alisema.
Alisema
jengo hilo likimalizika linaweza kuchukua watu 342, lakini hivi sasa lina watu
100, waliopo eneo la chini la ghorofa hilo, halina umeme wala maji.
Alisema
Muhimbili kuna jengo la Taasisi ya Tiba ya Mifupa ya Muhimbili (Moi), kuna
jengo la ghorofa sita lililoanza kujengwa miaka minne iliyopita, lakini mpaka
leo halijamalizika kutokana na mvutano kati ya Moi na mkandarasi anayetaka
kulipwa Sh9 bilioni.
“Wamechukua
wagonjwa wachache na kuwaweka ghorofa ya kwanza hadi ya tatu. Lina jenereta ila
haijafungwa. Hiyo ndiyo Tanzania,” alisema.
Alisema
ameshatoa maagizo kwamba ndani ya siku mbili wafanyakazi hao 70 waondolewe
kwenye jengo hilo linalotumika kama ofisi na badala yake viwekwe vitanda vya
wagonjwa.
“Sasa Waziri
wa Afya na Katibu Mkuu watajua watawatafutia wapi pa kuwapeleka. Wanaweza
kuwapeleka pale wizara ya Afya wakakae nao huko. Ndani ya siku mbili hizohizo
ofisi hiyo ijae vitanda na akina mama waliokuwa wanalala chini wahamishiwe
kwenye jengo hilo,” alisema.
Alisema ili
Tanzania isiwe ombaomba lazima viongozi wajifunze kutokukubali kulea makosa.
“Kama ni
majipu tutayatumbua kwelikweli. Likienda kichwani tutalitumbua, likienda
kifuani tutalitumbua, likienda mgongoni tutalitumbua ili mradi majipu yaishe na
Tanzania iende mbele,” alisema.
Tanzania
bila mapato haiwezekani.
Alisema Tanzania haiwezi kuendelea bila kuwa
na mapato yake.
“Wafanyabiashara
wamekuwa wakikwepa kulipa kodi. Mara ya kwanza tulipoanza kuchukua hatua
tulipata zaidi ya Sh1 trilioni, mwezi uliofuata tulipata Sh1.592 trilioni na
Januari tulikusanya Sh1.063 trilioni,” alisema.
Alisema
Serikali ya Awamu ya Tano inataka kuona fedha hizo zikiwahudumia wananchi
masikini.
“Zipo kejeli
nyingi, wanasema ni nguvu ya soda. Hata kama ni soda ukiweka gongo utalewa. Hii
ni soda ‘special’ ambayo tumedhamiria kufanya kazi kwa ajili ya Watanzania.
Haiwezekani nchi tajiri kama Tanzania tuwe ombaomba, inatakiwa iwe inaombwa
misaada,” alisema.
Aliwataka
Watanzania kujenga utamaduni wa kulipa kodi na kudai risiti kwa kila manunuzi
wanayoyafanya.
Kukwama kwa
mradi wa umeme.
Kuhusu mradi
wa umeme wa gesi wa Kinyerezi 2 uliokwama tangu mwaka 2012, alisema wafadhili
kutoka Japan walitoa dola 292 za Marekani na Serikali ya Tanzania ilitakiwa
kuchangia asilimia 15 ya fedha hizo.
Alisema
mradi huo utaingiza zaidi ya megawati 240 za umeme.
“Fedha hizo
tumezitoa na kampuni kutoka Japan imeshaanza kazi na mwezi ujao tunakwenda
kuweka jiwe la msingi. Mradi wa ujenzi wa barabara ya juu Dar es Salaam
mkandarasi ameshaanza kazi na fedha za awali ameshalipwa,” alisema.
Alisema
upembuzi yakinifu wa mradi wa barabara ya njia sita kutoka Dar es Salaam kwenda
Chalinze, umeshamalizika na kuna kandarasi zaidi ya 12 wameshaomba zabuni.
“Katika
kipindi hikihiki cha awamu ya tano itajengwa ili tuwe na barabara ya njia sita
kupunguza msongamano wa magari,” alisema.
Rais pia
alidokeza kuhusu mradi wa ujenzi wa daraja la urefu wa kilomita saba
litakalopita baharini kutoka ufukwe wa Coco hadi Hospitali ya Aga Khan, akisema
Serikali imeshapata zaidi ya Sh260 bilioni.
“Kuhusu
barabara ya Mbagala rangi tatu kuja mjini (Posta), nilikuwa nazungumza na
ubalozi wa Japan wapo katika utaratibu wa kutangaza tenda,” alisema.
Pia
alizungumzia ujenzi wa barabara za juu zitakayojengwa kwenye makutano ya
Ubungo.
Alisema
makutano hayo yatakuwa na ghorofa tatu ambazo zitakuwa na barabara zinazokutana
eneo hilo ili kuondoa tatizo la foleni.
“Benki ya
Dunia imekubali kutoka Sh67 bilioni kujenga interchange (mzunguko wa juu wa
barabara) ya ghorofa tatu pale Ubungo, nina uhakika watani zangu wazaramu
watakwenda pale kufunga ndoa,” alisema.
Kuifufua
ATCL.
Alisema Serikali ina mpango wa kufufua Shirika
la Ndege (ATCL), ambalo hivi sasa lina ndege moja lakini limeajiri wafanyakazi
200.
Alisema kwa
sasa wanakusanya fedha za kutosha ili kuweza kununua ndege aina ya Airbus yenye
uwezo wa kuchukua kuanzia abiria 120 na kuendelea, akisema bei yake ni takriban
Sh140 bilioni.
“Mkijipanga
mnaweza kuwa mnanunua ndege moja kila mwezi,”alisema.
Elimu bure.
Akizungumzia
changamoto ya elimu bure alisema wanafunzi walioanza darasa la kwanza nchini
mwaka huu ni 1,337,000, jambo ambalo alisema linaonyesha kuwa wananchi walikuwa
wakishindwa kuwapeleka watoto wao shule kwa sababu ya kukithiri kwa michango.
Alisema
changamoto zilizojitokeza baada ya Serikali kuanza kutoa elimu bure
watazimaliza, ikiwa ni pamoja na kutenga fedha nyingi zaidi kwa ajili ya
kuzipeleka katika shule.
Aliwashukuru
wananchi ambao wameanza kujitokeza kuchangia ujenzi wa madarasa na kumsifu Mkuu
wa Wilaya ya Kinondoni kwa kuendesha harambee ya kuchangia ujenzi wa shule.
Awashukia wakuu
wa mikoa na wilaya.
Dk Magufuli pia alizungumzia utendaji wa wakuu
wa wilaya na mikoa na wakurugenzi wao, akiwataka kutathmini hali ilivyo kwenye
shule na ofisi zao.
“Kama unajua
kujipima vizuri, ujitambue kuwa hutoshi kuwa kiongozi. Sijateua wakuu wa mikoa,
wakuu wilaya na wakurugenzi ili niendelee kuwachambua vizuri (waliopo) ni nani
anatosha na nani hatoshi,” alisema..
“Kutosha
kwao ni lazima wajipange watatatua vipi kero za wananchi. Lazima ifike mahali
viongozi tujue jukumu letu. Unapopewa jukumu la uongozi wewe ni mwakilishi wa
wanyonge.”
Huku
akiwataka Watanzania wa kada zote nao kujipima walichoifanyia nchi ndani ya
siku 100, alisema haingii akilini kiongozi kusimama na kusema chakula hakuna
wakati mvua inanyesha kila mkoa nchini.
“Kiongozi
umeshindwa hata kuhamasisha watu walime. Natoa wito kwa viongozi wenzangu.
Katika mkoa, wilaya au tarafa itakayokuwa haina chakula kwa mwaka huu ambao
mvua inanyesha, ajitambue hafai kuongoza katika nchi,” alisema.
Alisema
aliahidi kuwalipa wazee waliolitumikia taifa lakini jambo hilo haliwezekani
kama kutakuwa na vijana wanaoshinda mitaani bila kufanya kazi.
“Najua mkuu
wa mkoa wa Dar es Salaam, wakuu wa mikoa wenzako watakuuliza nitateua lini
wakuu wa mikoa na wilaya. Kwanza tarehe ya kuteua hawataijua na ninaendelea
kuwachambua,” alisema Magufuli.
“Lakini
angalau Makonda umeshajihakikishia walau utakuwepo ila na wewe usiende kulala,
endelea kufanya juhudi. “Ukipanda cheo watu wasikuonee wivu.”
Alisema
Makonda amejijengea heshima kubwa kwa kuhamasisha watu wa kada mbalimbali
kumaliza changamoto za kuongezeka wa wanafunzi, uhaba wa madarasa na madawati.
Kuhusu
changamoto za elimu bure, Rais alisema asilimia 80 ya viongozi wa Serikali ya
Awamu ya Tano wanaishi Dar es Salaam, akiwamo yeye, waziri mkuu, mawaziri,
makatibu wakuu na naibu spika.
“Wao wakitoa
milioni moja moja zinafika milioni 82 na zitabaki milioni 18, lakini kuna
Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na mimi. Tuigawane hii na kila mmoja achangie Sh6
milioni itimie Sh100 milioni na tutaileta kwenye uongozi wa mkoa wa Dar es
Salaam,” alisema.
Alisema kwa
mamlaka aliyonayo ataongeza Sh2 bilioni na kumtaka mkuu wa mkoa wa Dar es
Salaam kutozitumia vibaya, akitaka zigawanywe kwa kila wilaya ili zijengwe
shule za kutosha kufidia wanafunzi wanaokaa chini.
Afagilia
vyombo vya habari.
Kiongozi
huyo wa Serikali ya Awamu ya Tano pia alizungumzia vyombo vya habari ambavyo
alisema vimefanya kazi kubwa na kuisaidia Serikali.
“Hata sisi
huwa tunafuatilia. Mfano katika gazeti la Jamhuri waliweka michoro fulani mpaka
sisi (Serikali), tukajiuliza wamejuaje tunachotaka kukifanya?” alisema.
Hapa ni Video ya
Hotuba Ya Rais Magufuli.Msikilize Akiongea..''
|
No comments:
Post a Comment