Watumiaji
wengi wa huduma ya simu za mkononi wamekuwa wakilalamikia wizi wa pesa
unaofanywa na baadhi ya makampuni hayo, leo November 14,2014,katika kikao cha Bunge Dodoma
Serikali imesema inatambua kuhusu wizi
unaofanywa na baadhi ya makampuni ya simu za mkononi na kutoa tamko namna
ambavyo imejipanga kukabiliana na wizi wa aina hiyo.
Akitoa tamko
hilo Naibu Waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia Bw.January Makamba amesema
Serikali itaanzisha kituo maalum cha kushughulikia malalamiko hayo CCC,
kitakachokuwa kinasimamiwa na TCRA.
Akiuliza
swali kuhusiana na jinsi Serikali ilivyojipanga
kukabiliana na wizi huo Mbunge wa Konde Bw. Khatib Said Haji amesema; “…
Wizi huu unaofanywa na makampuni ya simu si wizi mkubwa kama ule wa
ESCROW.. ni wizi mdogo mdogo unaowaibia
Watanzania elfu tano elfu tatu lakini kwa ujumla wake, Mpemba aliyeko Konde
akiibiwa elfu tatu, Mnyamwezi wa Tabora elfu mbili, Ukizijumlisha ni mamilioni
ya shilingi wanaibiwa Watanzania… Leo watu hao elfu tatu elfu mbili unawaambia
wapeleke malalamiko yao, gharama hiyo umeikadiriaje hata mtu huyo akadai
malalamiko ya elfu tatu..”
“.. Hivi
serikali yenu makini imekuwa wapi muda wote mpaka kukiri kama Watanzania
wamekuwa wakiibiwa na bila wenyewe kujijua?, na bado hamna hatua mlizozichukua,
ni nani aliyeko nyuma ya pazia hili la kuibia Watanzania na ninyi mkaridhia ama
ni yale yaliyosemwa kama CCM ina fund katika wizi huu..?”- Khatib Said Haji.
Akijibu
swali hilo Naibu Waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia January Makamba
amesema; “…Napenda nikiri tatizo la wizi au dhuluma kwa wateja lipo na ndio
lililopelekea tukaweka hizi kanuni ambazo zinaweka adhabu na hatua za kuchukua
katika kuchukua katika kudhibiti wizi huo.. Licha ya utaratibu wa kawaida wa
kulalamika katika makampuni ya simu, kwa
sababu moja ya matakwa ya sheria ni kwamba kampuni za simu zinapaswa kuweka
utaratibu wa kuhudumia watekja wake, lakini tumebaini kwamba utaratibu huo una
matatizo, unaweza ukapiga simu muda
mrefu isipokelewe, unaweza kuambiwa usubiri na wakati unasubiri kulalamika pia
unakatwa..
Kwa hiyo
Serikali inafahamu hilo, pamoja na hatua tulizozichukua ni kuweka ule mtambo wa
kufuatilia mawasiliano ambao moja ya kazi yake sio kufuatilia tu mapato lakini
ubora wa mawasiliano.. Kwa kutambua kuwa makampuni ya simu haya wakati mwingine
yanachelewa wakati mwigine yanapuuza wateja, kituo hiki ambacho tunakianzisha
namba zake zitasambazwa kila mtu atakuwa nayo, kwa hiyo huna haja kusafiri
kufuatilia shilingi elfu mbili elfu tatu elfu tano. Kutakuwa na namba ambayo ni
bure kupiga..”- January Makamba.
“ Kila
utakapopiga kulalamika utapewa namba maalum ya lalamiko lako, na
lisiposhughulikiwa hata kitengo cha kampuni ya simu kutoshughulikia lalamiko
lako na yenyewe itakuwa sababu ya makampuni hayo kuadhibiwa..”- January
Makamba.
|
No comments:
Post a Comment